Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ameagiza wezi walioiba nguzo 147 katika uwanja wa ndege Moshi mkoani Kilimanjaro pamoja na fensi waya kurejesha mara moja.
Babu ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi mkoa.
Amesema kuwa serikali inaufanyia ukarabati uwanja huo wa ndege kwa maslahi ya nchi na kwamba waliofanya hivyo hawana uzalendo.
” Hatutafumbia macho vitendo hivi,” amesema.
Alisema kuwa, Bilioni 12.5 zimetolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ukarabati wa uwanja huo ambapo Bilioni 4 ni kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa uwanja huo.
Babu alisema kuwa, kabla Mkandarasi ambaye ni kampuni ya Rocktronic Ltd kukabidhi kazi ya ukarabati wapo watu wasio na nia njema wameiba nguzo 147 pamoja na kukata fensi waya na kuondoka nao.
“Waliofanya tukio hili ni Watanzania ambao hawana uchungu na hela zinazotolewa na serikali na nataka nguzo hizo pamoja na fensi waya kurejeshwa mara moja kwani serikali haitafumbia macho swala hili tutapambana na aliyepewa dhamana ya kulinda katika uwanja huo” Alisema Babu.
Akithibitisha kutokea kwa wizi huo, Mkurugenzi wa kampuni ya Rocktronic Ltd, Prajesh Chauhan alisema kuwa wamesharipoti swala hilo kituo cha Polisi Moshi kati kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

