Watoto wawili wa Kipalestina wameuawa baada ya shambulio la ndege isiyo na rubani ya Israel katika mji wa Bani Suheila, mashariki mwa Khan Younis, Gaza ya kusini. Mashuhuda wameiambia Al Jazeera kuwa bomu lilitupwa karibu na Shule ya al-Farabi, likiwalenga raia, na kusababisha vifo vya ndugu wawili, Juma na Fadi Tamer Abu Assi.
Kwa mujibu wa madaktari, watoto hao walifikishwa Hospitali ya Nasser wakiwa na majeraha mabaya na baadaye wakathibitishwa kufariki dunia.
Eneo lililoshambuliwa liko nje ya mstari unaoitwa Yellow Line, ambao unapaswa kuwa mpaka wa kurejea kwa majeshi ya Israel chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano ya Oktoba 10. Hii inaongeza idadi ya matukio ya uvunjaji wa makubaliano hayo.
Mapema leo, jeshi la Israel pia lilifanya mashambulizi ya ardhini, baharini na angani katika maeneo mbalimbali ya Gaza, likijeruhi raia kadhaa katika al-Qarara na mashariki mwa Gaza City na Rafah.
Tangu Oktoba 2023, mashambulizi ya Israel yamewaua karibu watu 70,000, wengi wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi zaidi ya 170,000. Hamas imetaka jumuiya ya kimataifa kuiwekea Israel presha kufuata makubaliano ya kusitisha mapigano.

