Binti Wa Jacob Zuma Ajiuzulu Katika Bunge La Afrika Kusini

Binti Wa Jacob Zuma Ajiuzulu Katika Bunge La Afrika Kusini

Duduzile Zuma Sambudla, Bintiye Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma, amejiuzulu katika Bunge la nchi hiyo kutokana na madai kwamba aliwarubuni Wanaume 17 kwenda kupigania Urusi nchini Ukraine.

Zuma-Sambudla alikuwa Mbunge katika Chama cha Upinzani cha Umkhonto weSizwe (MK) kinachoongozwa na baba yake.

Maafisa wa MK walisema alijiuzulu kwa hiari na kuondoka kwake katika Bunge la kitaifa na majukumu mengine yote ya umma kulianza mara moja.

Nathi Nhleko, Mratibu wa kitaifa wa chama cha MK, aliwaambia Waandishi wa habari kuwa MK hakihusika katika kuwarubuni Wanaume hao kwenda Urusi na kwamba kujiuzulu kwa Zuma-Sambudla sio kukiri makosa.

Siku ya Jumapili, Polisi walisema watamchunguza Zuma-Sambudla baada ya dadake wa kambo, Nkosazana Zuma-Mncube, kutoa ombi rasmi la uchunguzi dhidi yake na watu wengine wawili, akiwatuhumu kuhusika.

Zuma Sambudla alikuwepo kwenye mkutano na Waandishi wa habari lakini hakuzungumza, na hajajibu hadharani shutuma kutoka kwa dada yake wa kambo.

Serikali ya Afrika Kusini ilisema mwezi huu kuwa raia wake 17 walikwama katika eneo la Donbas nchini Ukraine baada ya kulaghaiwa kupigania vikosi vya mamluki kwa kisingizio cha kandarasi zenye faida kubwa za ajira.

Ilisema ilikuwa ikifanya kazi ya kuwarudisha nyumbani na kuchunguza jinsi walivyofika huko.

Comments

No comments yet. Why don’t you start the discussion?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *