
Sekta binafsi nchini imeanza kuchukua hatua madhubuti katika kuhamasisha mabadiliko ya kijani kupitia fedha ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuharakisha ajenda ya maendeleo endelevu ya taifa.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi Kongamano lililoandaliwa na Jukwaa la Wakurugenzi nchini ( CEOrt Roundtable) Tanzania na kuwakutanisha wadau kutoka sekta ya fedha, sekta binafsi, na taasisi za maendeleo za kimataifa kujadili mbinu bunifu na changamoto katika upanuzi wa fedha za kijani (green finance) ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu sanjari na kuimarisha mshikamano kati ya sekta za fedha katika kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia ubunifu wa kifedha, Mkurugenzi Mtendaji kutoka CEOrt, Santina Benson amesema kuwa uwezeshwaji wa kifedha ni msingi wa biashara endelevu na maendeleo ya kitaifa.

Amesema wakiwa kama jukwaa linalowakilisha sekta binafsi wanapaswa kuacha nadharia na kuhakikisha mitaji inawafikia wafanyabiashara walioko tayari kuwekeza katika ukuaji unaozingatia mazingira.
Amesema kuwa anatambua mafanikio yanayopatikana katika uwekezaji mbalimbali ikiwemo hati fungani (bonds) na utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa wadau wa maendeleo wakiwemo wakulima ambapo amesisitiza kuwepo kwa mazingira bora zaidi ya kuwezesha mabadiliko hayo.
Kwa upande wake Gabriel Lekundayo, Mkurugenzi kutoka Benki ya Biashara wa KCB Tanzania ambao pia ni miongoni mwa wadhamini wa kongamano hilo , amesema taasisi za kifedha zinajielekeza kwenye miradi yenye mwenendo wa tabianchi, hasa katika sekta za Kilimo na Miundombinu.
“Maoni kutoka katika kongamano hili yanaendana na vipaumbele vya hivi karibuni vya Serikali, hivyo sisi kama sekta ya fedha tutayafanyia kazi na kuyaunga mkono” Amesema Gabriel.
Peter Nalitolela, Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), alieleza maendeleo kupitia hati fungani, akisisitiza haja ya kuongeza ushiriki na kuimarisha mifumo ya taasisi ya kifedha ili kuwafikia watu wengi zaidi.
Naye Innocent Yonazi, Mkuu wa Mahusiano na Wawekezaji wa Benki ya NMB, alisisitiza umuhimu wa fedha jumuishi, akitaja nafasi muhimu ya wanawake, vijana, na jamii zilizo pembezoni katika kujenga uchumi thabiti wa kijani.
“Kuchelewesha hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutazidisha umaskini na ukosefu wa chakula,” alionya.

CEOrt inaendelea kujitolea kuhamasisha uongozi wa sekta binafsi katika kushiriki ukuaji wa uchumi kupitia —mpango unaolenga kutafsiri sera za taifa za tabianchi kuwa uwekezaji wenye tija kutoka sekta binafsi.-
