Bodi ya Ligi imeeleza utaratibu mpya wa matumizi ya mfumo wa FVS (Football Video Support) katika michezo, ambapo kila benchi litapewa kadi mbili maalum za kuomba marejeo ya tukio kwa msaada wa mfumo huo.
Akizungumza kuhusu utaratibu huo, CEO wa Bodi ya Ligi, Cornel Barnabas, amesema jumla ya kadi nne zitatumika katika mchezo, huku kila benchi likipewa kadi mbili ambazo zitatumika pale linapoona kuna tukio linalohitaji kuangaliwa upya ili kuhakikisha haki inatendeka.
Amesema benchi litakapohitaji FVS, litapaswa kuinua kadi yake juu kuashiria kwa mwamuzi kwamba linaomba tukio hilo lifanyiwe mapitio. Baada ya hapo, mwamuzi ataelekea kwenye mfumo wa FVS kwa ajili ya kupitia tukio husika.Barnabas amesisitiza kuwa kuna muda maalum wa kuwasilisha ombi hilo, ambapo benchi linatakiwa kuinua kadi ndani ya sekunde 60 tangu tukio litokee.
Ameongeza kuwa ombi hilo halitakubalika endapo benchi litachelewa na kusubiri tukio kupita kabla ya kuonesha kadi, hatua inayolenga kuhakikisha matumizi ya FVS yanafanyika kwa wakati na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

