Serikali ya Gabon imetangaza kusimamisha shughuli za timu yake ya taifa, ‘The Panthers’, kuvunja benchi la ufundi, na kuwaengua kikosini mastaa Pierre-Emerick Aubameyang na Bruno Ecuele Manga. Hatua hiyo kali imechukuliwa kufuatia matokeo mabovu ya timu hiyo katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) inayoendelea nchini Morocco.
Waziri wa Michezo nchini humo, Simplice-Desire Mamboula, alitangaza uamuzi huo kupitia televisheni ya taifa baada ya Gabon kushika mkia katika kundi lake bila alama yoyote. Waziri Mamboula aliyataja matokeo hayo kuwa ni “utendaji wa kiaibu” uliolilazimu taifa kuchukua hatua za dharura hadi hapo itakapotangazwa tena.
Gabon, iliyokuwa chini ya kocha Thierry Mouyouma, ilitupwa nje ya mashindano mapema baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza dhidi ya Cameroon na Mozambique. Katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya mabingwa watetezi, Ivory Coast, Gabon walipoteza kwa mabao 3-2 licha ya kutangulia kwa mabao 2-0, jambo lililozidisha hasira za serikali na wadau wa soka nchini humo.

