Jeshi la Marekani limefanya mashambulizi ya kijeshi nchini Venezuela, huku milipuko ikitikisa mji mkuu, Caracas, na majimbo jirani ya Miranda, Aragua, na La Guaira. Shambulio hilo limekuja baada ya miezi kadhaa ya vitisho kutoka kwa Rais Donald Trump dhidi ya serikali ya Rais Nicolas Maduro, hali iliyompelekea Maduro kutangaza hali ya hatari na kuhamasisha vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo.
Mashambulizi hayo yalianza majira ya saa nane usiku na kudumu kwa takriban dakika 90, ambapo moshi mweusi na miale ya moto vilionekana angani huku kukiripotiwa kukatika kwa umeme katika maeneo ya kusini mwa Caracas karibu na kambi kubwa ya kijeshi. Serikali ya Venezuela imetoa tamko ikilaani shambulio hilo, ikidai kuwa lengo la Marekani ni kupora rasilimali za mafuta na madini, ikisisitiza kuwa Washington “haitafanikiwa.”
Rais Trump amekuwa akishinikiza Maduro kuondoka madarakani, akidai kuwa alichukua madaraka kwa udanganyifu katika uchaguzi uliopita. Kabla ya mashambulizi haya, Marekani ilikuwa imeweka tayari meli za kivita na ndege za kijeshi katika Bahari ya Caribbean, huku Trump akituhumu serikali ya Maduro kuhusika na biashara ya dawa za kulevya—tuhuma ambazo Venezuela imezikanusha vikali.
Ingawa Ikulu ya Marekani imekataa kutoa maelezo ya kina, mashambulizi haya yanakuja wiki moja tu baada ya Trump kutangaza kuwa Marekani ilishambulia maeneo yanayotumika kupakia dawa za kulevya nchini humo. Mataifa mengi yameanza kulaani hatua hizo yakizitaja kama mauaji ya kiholela na ukiukwaji wa sheria za kimataifa, huku hali ya taharuki ikizidi kutanda nchini Venezuela.

