Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amepanda ndege ya kijeshi kabla ya kuondoka kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa King Abdulaziz huko Jeddah, Saudi Arabia, Machi 12, 2025.
Rubio anasafiri kuelekea Canada kwa ajili ya mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa G7.
Mawaziri wa mambo ya nje kutoka kundi la G7 la mataifa yanayoongoza kiviwanda wanatazamiwa kukusanyika kwa siku kadhaa za mazungumzo mjini Quebec, Canada, ikiwa ni pamoja na mikutano inayoangazia uungaji mkono kwa Ukraine katika vita vyake dhidi ya uvamizi wa miaka mitatu wa Urusi.
Mazungumzo hayo yanafuatia uamuzi wa Marekani wa kurejesha ushirikiano wa kijasusi na usaidizi wa kiusalama kwa Ukraine, baada ya maafisa wakuu kutoka nchi hizo mbili kukutana mjini Jeddah.
Baada ya karibu saa nane za mazungumzo, Ukraine ilitangaza Jumanne utayari wake wa kukubali pendekezo la Marekani la “kusitisha mapigano mara moja kwa muda wa siku 30” katika vita na Urusi, ikisubiri idhini ya Kremlin.

