Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mshauri wa Rais wa Tanzania kuhusu Masuala ya Afya, Pro. Mohamed Janabi amechanguliwa kuwa Mkurugenzi mpya wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika, nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Faustine Ndugulile aliyefariki Dunia.
Prof. Janabi ameshinda nafasi hiyo kwenye uchaguzi uliofanyika leo Mei 18, 2025 Geneva kwa ajili ya kuziba nafasi ambayo iliachwa wazi na Dkt. Ndugulile ambapo Prof Janabi alikuwa Mgombea pekee kutoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara.
Wagombea wengine wanne wametokea nchi za Afrika Magharibi akiwemo Dkt. N’da Konan Michel Yao (Ivory Coast), Dkt. Dramé Mohammed Lamine (Guinea), Dkt. Boureima Hama Sambo (Niger) na Prof. Mijiyawa Moustafa wa Togo.
Kabla ya kuchaguliwa, Prof. Janabi, pamoja na mambo mengine aliahidi uboreshaji wa huduma za afya na kuweka mkazo zaidi kwenye uboreshaji wa huduma za afya ngazi ya msingi.
Prof. Janabi alisema atasimamia upatikanaji wa rasilimali fedha za kuwezesha kugharamia upatikanaji wa huduma bora za afya.
Amesema atasimamia utayari wa nchi wanachama katika kukabiliana na majanga pamoja na dharura za afya.
Pia ameongelea kuhusu kuboreha huduma za afya ya uzazi mama na mtoto.

