Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika Dk Faustine Ndugulile amesema kuwa ataanza rasmi majukumu yake mwezi Machi 2025.
Hii amesema inatokana na utaratibu wa mashirika ya kimataifa ambapo kazi ataanza baada ya miezi 6.
Akiongea bungeni kwa mara ya kwanza toka ashinde nafasi hiyo, Mh Ndugulile pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan wasaidizi wake pamoja na mhimili wa bunge kwa ushirikiano wao katika kumsaidia kupata nafasi hiyo.
Pia amesema kuwa katika uongozi wake ataweka vipaumbele katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya barani Afrika na kuhakikisha bara hilo linajiandaa vema kukabiliana na majanga makubwa ya kiafya yanayojitokeza kama Uviko 19 pamoja na Mpox.
Dk Ndugulile ambaye ni Mbunge wa Kigamboni ameyasema hayo wakati anatoa salamu za shukrani mara baada ya kushinda nafasi hiyo juma moja lililopita bungeni jijini Dodoma leo Septemba 3, 2024.

