Eberechi Eze amefunga bao lake la kwanza la Ligi ya Premia akiwa na Arsenal na kuipa ushindi wa 1-0 dhidi ya klabu yake ya zamani Crystal Palace siku ya Jumapili.
Eze alifunga bao lake hilo la kwanza mwishoni mwa kipindi cha kwanza kwenye uwanja wa Emirates na kuhakikisha Arsenal wanatumia kikamilifu vipigo vya apinzani wao Liverpool na Manchester City katika vita ya kuwania taji msimu huu.
Kiungo huyo wa kati wa Uingereza alikuwa ameifungia The Gunners mara moja pekee katika mechi 10 zilizopita katika michuano yote tangu awasili kutoka Palace kwa kitita cha pauni milioni 60 ($79 milioni) mwezi Agosti.
Wakiwa wamemaliza kama washindi wa pili kwa miaka mitatu iliyopita, ushindi wa saba wa Arsenal kutoka katika mechi tisa za ligi uliongeza hisia kwamba huu unaweza kuwa msimu wao hatimaye kumaliza ukame wao wa ubingwa.
Kikosi cha Mikel Arteta kiko pointi nne mbele ya Bournemouth iliyo nafasi ya pili na, kikubwa zaidi, sita mbele ya Manchester City na saba mbele ya Liverpool.
Kipigo cha 3-2 cha Liverpool dhidi ya Brentford siku ya Jumamosi kiliwaacha mabingwa hao watetezi wa taji katika misukosuko baada ya kushindwa kwa mara ya nne mfululizo kwenye ligi.

