Kinda wa Real Madrid anayekipiga kwa mkopo Lyon, Endrick, ameonyesha kiwango cha hali ya juu baada ya kufunga bao na kutoa asisti katika ushindi wa kushtukiza wa 2-1 dhidi ya Paris Saint-Germain usiku wa Jumapili. Ushindi huo uliopatikana katika dimba la Parc des Princes umetoa pigo kwa PSG na kufungua milango kwa Lyon kuwania nafasi ya nne bora na ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) msimu ujao.
Licha ya PSG kuingia uwanjani wakiwa na morali ya kuiondoa Liverpool kwenye UCL wiki iliyopita, walijikuta wakishitukizwa mapema dakika ya sita pale Endrick alipounganisha pasi ya Afonso Moreira. Dakika 12 baadaye, Endrick alirudisha fadhila kwa kumtengenezea Moreira bao la pili, na kuiacha timu ya Luis Enrique ikiwa na bumbuwazi.
PSG walipata nafasi ya kurejea mchezoni baada ya Lucas Hernandez kufanyiwa madhambi na Ainsley Maitland-Niles ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, mshambuliaji Goncalo Ramos alishindwa kutumia nafasi hiyo baada ya mkwaju wake wa penalti kuokolewa kwa urahisi na kipa wa Lyon, Dominik Greif.
Hali ilizidi kuwa mbaya kwa PSG kipindi cha kwanza baada ya kiungo wao, Vitinha, kulazimika kutoka nje kutokana na jeraha. Licha ya Luis Enrique kuwaingiza wachezaji nyota kama Khvicha Kvaratskhelia na Ousmane Dembele kipindi cha pili, Lyon walisimama imara kulinda ushindi wao.
PSG walipata bao la kufutia machozi katika dakika za majeruhi kupitia kwa Kvaratskhelia, lakini haikutosha kuzuia kipigo hicho nyumbani.

