
Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mheshimiwa Farida Mgomi amewaasa wananchi kuwa na utamaduni wa kuwashika mkono na kutoa misaada kwa makundi yenye uhitaji maalumu katika jamii.
Amesema kwa kufanya hivyo watakuwa wameigusa jamii na kuipa faraja katika nyakati zote.
Akizungumza wakati wa hafla ya kutoa misaada katika kituo cha Watoto yatima cha Hospitali ya Isoko kilichopo Kata ya Kafule wilayani Ileje iliyonogeshwa na kikundi cha Wandali waishio Tunduma, Dc Mgomi amesema kuigusa jamii yenye uhitaji maalumu ni kitendo cha kujipatia baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu hivyo jamii inatakiwa kufanya hivyo.

” Tunahitaji kuwa karibu na watu wenye mahitaji nyakati zote, zikiwemo nyakati za Sikukuu ili nao kuwapa furaha na amani moyoni mwao,”, amesema mheshimiwa Mgomi.
Naye Mbunge wa Viti maalumu Mhe Stella Fiyao ambaye aliambatana na kikundi cha Wandali katika hafla hiyo, ameahidi kuwa kikundi hicho kitaendelea kuigusa na kuipa faraja jamii kupitia misaada mbalimbali watakayokuwa wakiitoa na litakuwa zoezi endelevu la kuigusa jamii.

Misaada uliyokabidhiwa ni pamoja na vyakula na mahitaji mbalimbali mengine kama vile mafuta, taulo za kike, mashuka, sabuni za kuogea na kufulia, sukari, chumvi, nguo, madaftari na kalamu ambapo kwa ujumla msaada huo umegharimu takiribani shilingi million Tatu.
