Chalamila atoa wiki mbili Machinga kufungua njia soko la Kariakoo

Chalamila atoa wiki mbili Machinga kufungua njia soko la Kariakoo

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa muda wa wiki mbili kwa uongozi wa wafanyabiashara wadogo (machinga) wa eneo la Kariakoo kuhakikisha wanafungua njia zinazozunguka soko hilo ili kuruhusu magari yanayopeleka bidhaa sokoni hapo kuingia kwa urahisi.

Amesema kuwa ujenzi wa soko hilo ambalo liliungua moto umekamilika kwa asilimia 98, hivyo kuwa tayari kwa ajili ya biashara.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Mei 30, 2025, Chalamila amesema kwamba ni lazima maandalizi yawe yamekamilika ifikapo muda wa uzinduzi rasmi.

“Natoa muda wa wiki mbili ili uongozi wa Kariakoo na wafanyabiashara ndogondogo wawaeleze kuhusu dhamira ya Serikali na namna ya kufungua njia ili kila mmoja abebe mzigo huu wa kufanikisha shughuli hii. Tusipofanya hivyo, tutajikuta tunabaki na soko lisilo na tija licha ya uwekezaji mkubwa uliokwisha kufanyika,” amesema Chalamila.

Ameongeza kuwa Serikali haitakubali kuona uwekezaji mkubwa uliofanyika katika ujenzi wa soko hilo ukikwamishwa na baadhi ya watu kushikilia maeneo kiholela. Aidha, amewataka viongozi wa wafanyabiashara hao kutoa elimu na ushawishi kwa wanachama wao ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa amani na ufanisi.

Soko jipya la Kariakoo linatajwa kuwa la kisasa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki, likitarajiwa kuongeza ufanisi wa biashara jijini Dar es Salaam na kutoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa.

Comments

No comments yet. Why don’t you start the discussion?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *