Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia mkutano wake na waandishi wa habari kimelaani jeshi la Polisi kukamata viongozi wake hivi karibuni.
Viongozi hao walikamatwa wakati wa maadhilisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyoratibiwa na Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) Jijini Mbeya.
Akizunguza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mbowe amesema kuwa jeshi hilo linatumia nguvu kubwa pasipo na msingi wowote.
Kauli hiyo inakuja baada ya viongozi waandamizi wa chama hicho akiwemo Mbowe mwenyewe kukamatwa na jeshi hilo mkoani Mbeya hivi karibuni kwa kufanya mkutano bila utaratibu, kwa mujibu wa Polisi.
Katika mkutano huo, Mbowe amesema kuwa wanakusudia kufungua kesi mahakamani kwa kile walichodai kunyimwa uhuru wa kukusanyika kwa mujibu wa sheria.
Mbowe amesema kuwa wana haki ya kufanya hivyo na badala yake polisi wanatakiwa kulinda usalama na sio vinginevyo.
Kukamatwa kwa viongozi hao kulilaaniwa na watu mbalimbali, huku Polisi wakidai kuwa kumetokana na kauli zilizoashiria uvunjifu wa amani na vurugu.

