Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan amesema chama hicho kimependekeza kufanya mambo yake kisasa kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia kwa kufanya mikutano yake kisasa.
Akizungumza katika mkutano mkuu maalumu wa CCM Taifa leo Mei 29, 2025 Jijini Dodoma, Rais Samia amesema hilo ni pendekezo la kwanza ambalo wajumbe wa mkutano huo watatakiwa kulijadili.
“Tunatakiwa kuenda sambamba na ukuaji wa teknolojia ili kuwafikia watu wetu kwa urahisi,” amesema.
” Tumefunga mitambo ya kuweza kuwasiliana na mikoa na wilaya ili kurahisisha utendaji wa kazi,”
“Tumekuja na wazo la E-meetings (Mikutano ya kimtandao) ambayo Idara ya Oganaizesheni inapendekeza vikao vifuatavyo vifanyike kwa njia ya mtandao…Kikao cha kwanza ni Sekretarieti ya Wilaya, kamati ya siasa ya wilaya, Sekretarieti ya mkoa, Kamati ya siasa ya mkoa, Sekretarieti ya kamati maalumu ya halmashauri kuu ya CCM Taifa, Sekretarieti ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Kamati Maalumu ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Halmashauri kuu ya CCM Taifa na Mkutano Mkuu wa Taifa.” amesema Rais Samia
Ameongeza kuwa mikutano hiyo itafanyika kwa njia ya mtandao endapo tu kutakuwa na ulazima na kwamba ile ya ngazi ya wilaya na mkoa itafanyika kwa idhini ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa.
Rais Samia ameelekeza hilo lifanyike ili kuepusha kutumika vibaya kwa mitandao kupitia vikao hivyo.

