Hali ya mambo imechafuka katika klabu ya Celtic baada ya mashabiki wenye hasira kukusanyika nje ya uwanja wa Celtic Park siku ya Jumamosi, wakidai mabadiliko ya haraka uongozini kufuatia kipigo cha fedheha cha 3-1 mikononi mwa mahasimu wao wakubwa, Rangers. Kipigo hicho kimeiacha Celtic ikilingana pointi na Rangers katika nafasi ya pili, zote zikizikimbiza Hearts wanaoongoza ligi, hali ambayo mashabiki wa Celtic haijaizoea kutokana na kutawala soka la Scotland kwa miaka ya hivi karibuni.
Mchezo huo ulianza kwa matumaini baada ya Yang Hyun-Jun kuifungia Celtic bao la uongozi kipindi cha kwanza, lakini mambo yalibadilika ghafla Rangers waliporejea kwa kasi na kufunga mabao matatu kupitia kwa Youssef Chermiti (mabao mawili) na Mikey Moore. Hali ya chuki ilitanda uwanjani huku mashabiki wakianza kuzomea, wengine wakiondoka mapema na wengi wakielekeza lawama kwa kocha Wilfried Nancy na bodi ya wakurugenzi kwa ukosefu wa uwekezaji kwenye usajili.
Kocha Nancy, ambaye ameshinda mechi mbili tu kati ya nane tangu achukue mikoba mwezi uliopita, anakabiliwa na shinikizo kubwa huku kikiwa hakuna mechi hata moja ambayo timu yake imeweza kuzuia nyavu zake kuguswa (clean sheet). Hata hivyo, Nancy amesisitiza kuwa bado anaungwa mkono na uongozi na ana imani ya kubadili mwenendo wa timu, akisema anaelewa machungu ya mashabiki lakini anahitaji muda zaidi wa kufanya kazi na kikosi hicho.
Pamoja na Celtic kushinda mataji manne yaliyopita ya Ligi Kuu ya Scotland, mashabiki wamekuwa wakilalamikia kudorora kwa timu hiyo katika mashindano ya Ulaya na kile wanachokiita uwekezaji mdogo kutoka kwa bodi, jambo ambalo limefikia kilele chake baada ya kipigo hiki cha “Old Firm”.

