Jeshi la Polisi Mkoani Geita Kupitia Kamanda wa Polisi SACP Safia Jongo ametoa tathimini ya hali ya mwenendo wa wa ufukuaji kufuatia ajali ya kutitia kwa Mgodi Mdogo wa dhahabu wa Msasa huku akiuhakikishia umma kuwa hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa katika tukio hilo.
Amesema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Wananchi pamoja na Wachimbaji wadogo wa Mgodi huo katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Mgodini hapo Machi 30 , 2026 ambapo Kamanda Jongo amesema kuwa hali ya Usalama imedhibitiwa kikamilifu katika Mgodi baada ya kutitia.
Aidha Kamanda SACP Jongo ametumia pia Mkutano huo kuhoji Wananchi pamoja na Wachimbaji kwa mtu yoyote mwenye taarifa za ndugu au mfanyakaji mwenzake kupotea au kutoonekana tangu kutokea kwa hitilafu hiyo, ambapo Wananchi waliohojiwa katika eneo hilo nao wamekiri kwa pamoja kuwa hakuna mtu aliyekosekana wala kupata madhara kutokana na tukio hilo .
“Ni jambo la kumshukuru Mungu kuwa jitihada zetu za ufukuaji zimethibitisha kuwa hakuna aliyepata madhara. Tunapaswa kuwa makini na taarifa zisizo rasmi zinazoeneza hofu. Kitaalamu tumefanya kila linalowezekana kujiridhisha na usalama wa eneo hili,” amesema Kamanda SACP Kamanda Jongo.
Ikumbukwe kuwa zoezi la ufukuaji na ukaguzi wa eneo la tukio linatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya wananchi, Jeshi la Polisi, Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Ofisi ya Madini.
Afisa Madini wa Mkoa wa Kimadini Mbogwe, Joseph Mrimi, ameeleza kuwa hatua za ufukuaji zimefikia sehemu nzuri na amesema kuwa pindi zoezi hilo litakapokamilika, ukaguzi wa kina wa kiufundi utafanyika mara moja ili kuruhusu shughuli za uzalishaji kuendelea katika mazingira salama.
Naye Kaimu Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, ASF Keneth Mwakasitu, amewahakikishia Wananchi kuwa timu za uokoaji zipo eneo la tukio na zinaendelea na kazi kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha eneo lote linakuwa salama kwa matumizi ya kibinadamu.

