Rais wa Donald Trump ameonya kuwa wananchi wa Marekani wanapaswa kujiandaa kwa ongezeko la bei ya mafuta katika kipindi cha karibu, kufuatia mvutano wa kijeshi unaoendelea kati ya Marekani na mshirika wake Israel dhidi ya Iran.
Akizungumza kuhusu hali hiyo, Trump alisema kuwa kupanda kwa gharama za nishati ni “bei ndogo ya kulipa” ili kulinda maslahi ya kimkakati na usalama wa washirika wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.
Onyo hilo linakuja wakati ambapo masoko ya kimataifa ya mafuta yanaendelea kuyumba kutokana na hofu ya kukatizwa kwa usambazaji wa mafuta kutoka ukanda huo muhimu duniani. Wachambuzi wa uchumi wanaeleza kuwa mzozo huo unaweza kusababisha athari kubwa kwa gharama za maisha, hususan katika sekta ya usafirishaji na uzalishaji.
Wananchi wa Marekani pamoja na nchi nyingine duniani wanatarajiwa kuhisi athari za moja kwa moja kupitia kupanda kwa bei za mafuta na bidhaa nyingine zinazotegemea nishati hiyo.
Serikali ya Marekani bado haijatoa maelezo ya kina kuhusu muda wa mzozo huo, huku juhudi za kidiplomasia zikitajwa kuendelea ili kupunguza mvutano huo unaozidi kuongezeka.

