TANZANIA KUTUMIA FURSA ZA IMF NA BENKI YA DUNIA KUKUZA UCHUMI

TANZANIA KUTUMIA FURSA ZA IMF NA BENKI YA DUNIA KUKUZA UCHUMI

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amesema Tanzania imejipanga kutumia mikutano ya mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, inayofanyika Bangkok, Thailand, Oktoba 12 hadi 18, 2026 kuimarisha uchumi na kupata rasilimali za miradi ya maendeleo.

Amesema ushiriki huo utatumika kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu na viongozi wa taasisi hizo, kuhamasisha ufadhili na kuendeleza ajenda za maendeleo ya Taifa.

Amebainisha kuwa Serikali imewasilisha orodha ya awali ya miradi inayotarajiwa kufadhiliwa kupitia mzunguko wa 21 wa Mfuko wa Maendeleo wa Kimataifa wa Benki ya Dunia (IDA 21), kwa lengo la kupata fedha za kutekeleza miradi ya kipaumbele.

Aidha, Tanzania inaendelea kupanua ushirikiano na wadau wa maendeleo, ikiwemo mashirika ya ukadiriaji wa mikopo ya Moody’s na Fitch, pamoja na kutafuta wakopeshaji wapya ili kuongeza upatikanaji wa fedha na kuimarisha imani ya wawekezaji.

Kwa upande wake, Balozi wa Heshima wa Tanzania nchini Thailand, Florean Rwehumbiza, amesema ofisi yake inaendelea kutangaza utalii wa Tanzania katika nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia na kuimarisha ushirikiano katika biashara na huduma za afya.

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazowapeleka wagonjwa wengi Thailand kwa matibabu, huku takwimu zikionyesha Watanzania wametumia takribani baht milioni 150 kuanzia Desemba 2025 hadi Juni 2026 kwa huduma hizo.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Ali Hassan Omar, ameipongeza Wizara ya Fedha kwa kulishirikisha Bunge katika maandalizi ya mikutano hiyo, akieleza kuwa upatikanaji wa rasilimali ni muhimu katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Comments

No comments yet. Why don’t you start the discussion?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *