Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika Simba leo usiku wanashuka dimbani nchini Morocco katika mechi ya fainali ya mkondo wa kwanza ya michuano hiyo dhidi ya wenyeji RS Berkane.
Maandalizi kuelekea mechi hiyo yamekamilika ambapo Simba wameahidi kufa na kupona kupata matokeo ugenini ili kazi iwe nyepesi katika mechi ya mkondo wa pili nchini.
Wakati kocha wa Simba Fadlu Davids akiwa na matumaini ya ushindi, kocha Mouin Chaabani wa RS Berkane ya Morocco amesema mechi hiyo haitakuwa rahisi kwa pande zote mbili.
Raia huyo wa Tunisia mwenye umri wa miaka 43 aliwaambia waandishi wa habari kabla ya mechi ya mkondo wa kwanza mjini Berkane usiku wa leo Mei 27,2025 kuwa mechi hiyo mpaka sasa ipo wazi kwa Berkane na wageni wao Simba.
“Simba wana historia ya kujivunia katika mashindano haya na wanastahili kufika fainali, wamepata haki ya kuwania ubingwa,”
“Hata hivyo, mradi tutaweka juhudi na kujiandaa ipasavyo, hakuna sababu kwa nini hatuwezi kuleta kombe Morocco.” Chaabani, ambaye alishinda mataji saba kama mkufunzi wa Esperance katika nchi yake, anatafuta mataji matatu na Berkane katika kampeni hii.
Orange Boys tayari wameshinda ligi ya Morocco kwa mara ya kwanza tangu ianzishwe mwaka wa 1938, wametinga hatua ya 16 bora katika kombe la taifa, na wanatafuta utukufu wa Afrika.
Berkane wanaonekana kwenye fainali ya tano ya Kombe la Shirikisho katika misimu saba.
Walishinda 2020 na 2022 na walikuwa washindi wa pili mnamo 2019 na 2024.
Simba kwa upande wao wanafuta historia kwa mara ya kwanza endapo watatwaa taji hilo.
Je, una tabiri nini mechi hii?

