Serikali imeeleza utayari wake wa kushirikiana kwa karibu na wadau wa sekta binafsi, likiwemo Jukwaa la Watendaji Wakuu nchini ( CEO Roundtable of Tanzania- (CEOrt) ili kuhakikisha huduma ya afya kwa wote (Universal Health Coverage) inapatikana kwa Watanzania wote.
Mganga Mkuu Afisa Mkuu , Dkt. Grace Magembe alitoa kauli hiyo wakati wa chakula cha jioni ( Iftar Networking Dinner) kilichoandaliwa na JUkwaa hilo katika Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi Serikali, sekta ya biashara, watunga sera, washirika wa maendeleo na wadau wa afya walikutana kujadili nafasi ya sekta binafsi katika kuimarisha mfumo wa afya nchini katika hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam chini ya kauli mbiu “Afya kama Uwekezaji: Hoja ya Kibiashara kwa Afya kwa Wote.”
Dkt. Magembe alisema Serikali inatambua umuhimu wa ushirikiano na sekta binafsi katika kuendeleza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance Act) pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini kote.
“Serikali iko tayari kushirikiana na sekta binafsi kupitia majukwaa kama CEO Roundtable of Tanzania ili kuhakikisha bima ya afya kwa wote inakuwa halisi kwa kila Mtanzania,” alisema.
Alieleza kuwa ajenda ya Serikali ya kufanikisha huduma ya afya kwa wote inaongozwa na nguzo kuu tatu ambazo ni kupanua upatikanaji wa huduma za afya, kuboresha uwezo wa wananchi kumudu gharama za matibabu, pamoja na kuhakikisha utoaji wa huduma bora za afya.
“Bima ya Afya kwa Wote inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila kukumbana na changamoto za kifedha. Miundombinu na huduma za afya zinaendelea kupanuliwa, lakini mfumo wa bima unahakikisha gharama hazizuii wananchi kupata huduma wanazohitaji,” alisema Dkt. Magembe.
Kwa mujibu wa Afisa Mkuu huyo wa Tiba, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mfumo wa afya katika kipindi cha muongo mmoja uliopita. Alisema takribani asilimia 80 hadi 85 ya Watanzania sasa wanaweza kufika kwenye kituo cha afya ndani ya umbali wa kilomita tano.
Aidha, alitaja uwekezaji unaoendelea katika teknolojia za uchunguzi wa magonjwa, huduma za dharura pamoja na mafunzo ya kitaalamu kwa madaktari bingwa kuwa umeimarisha uwezo wa mfumo wa afya nchini.
Dkt. Magembe alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi unaendelea kuwa muhimu katika kuendeleza mageuzi ya sekta ya afya na kuboresha utoaji wa huduma nchini.
“Rasilimali muhimu zaidi kwa taasisi yoyote ni watu wake. Tukiiwekeza katika rasilimali watu na kulinda afya ya wafanyakazi wetu, tunaimarisha uzalishaji, ustahimilivu wa uchumi na maendeleo ya muda mrefu ya taifa,” aliongeza.
Akiwasilisha hotuba kuu, Afisa Mtendaji Mkuu Strategis Insurance Group Tanzania Limited, Dkt. Flora Minja alisema mifumo imara ya afya ni muhimu si tu kwa ustawi wa jamii bali pia kwa uendelevu wa biashara na maendeleo ya uchumi.
Alisema kampuni nyingi sasa zinatambua umuhimu wa kimkakati wa kuwekeza katika afya ya wafanyakazi wao.
“Makampuni hufanikiwa pale watu wake wanapokuwa na afya njema. Ugonjwa unapovuruga nguvu kazi, mashirika hukumbana na changamoto za uzalishaji, kushuka kwa ufanisi na ugumu wa kuhifadhi wafanyakazi wenye ujuzi,” alisema Dkt. Minja.
Aliongeza kuwa kuimarisha huduma za bima ya afya kunaweza kusaidia makampuni kudumisha utulivu wa nguvu kazi huku yakichangia maendeleo ya taifa.
Dkt. Minja pia alionya kuwa gharama za huduma za afya zinaendelea kuongezeka duniani kwa kasi kubwa kuliko mfumuko wa bei wa kawaida, akisisitiza umuhimu wa kupanua huduma za bima na kuimarisha mifumo ya kinga ya afya ili kuhakikisha huduma za afya zinabaki kuwa nafuu na endelevu kwa waajiri na wafanyakazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CEO Roundtable of Tanzania , *Bi. Santina Majengo Benson, alisema sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kusaidia vipaumbele vya afya vya taifa kupitia programu za afya mahali pa kazi, bima za afya na ushirikiano unaoimarisha mfumo mzima wa afya.
Alisema majukwaa kama ‘ Ifter Networking Dinner yanayoandaliwa na jukwaa hilo hutoa fursa kwa viongozi wa biashara na watunga sera kubadilishana mawazo, kujenga ushirikiano na kutambua njia za vitendo ambazo sekta binafsi inaweza kutumia kuchangia kuboresha matokeo ya afya nchini.
CEO Roundtable of Tanzania inasisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwa jukwaa la majadiliano, utetezi na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kusaidia safari ya Tanzania kuelekea kufanikisha huduma ya afya kwa wote kwa kuzingatia pia mkakati wa Dira wa 2050.

