Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametangaza mkataba kati ya Tanzania na Angola wa kuunganisha shughuli za usafirishaji kutoka Bahari ya Hindi hadi Bahari ya Atlantiki kwa kutumia reli itakayopita Zambia na DRC.
Uunganishaji huu utahusisha Reli ya Benguela ya Angola na ile ya Tanzania-Zambia (TAZARA) inayofika kwenye bandari ya Dar es Salaam.Mpango huo utaunganisha kwa pamoja Ukanda wa Lobito uliopo Atlantiki na Ukanda wa Kati unaoishia kwenye Pwani ya Bahari ya Hindi.
Hata hivyo, Rais Samia hakubainisha muda sahihi au tarehe ya kukamilika kwa mradi huo alipokuwa akiongea na wanahabari.
Mnamo mwaka 2025, Serikali ya China iliingia mkataba wa $1.4 bilioni na nchi za Zambia na Tanzania kwa ajili ya kufanya ukarabati wa TAZARA, reli iliyofadhiliwa na China miaka ya 1970 kurahisisha usafirishaji wa shaba na mafuta.
Hivi karibuni, kampuni ya ujenzi ya Webuild kutoka Italia imetangaza kupata kandarasi ya kujenga kipande cha Reli ya Ukanda wa Lobito nchini Zambia.
Kwa muda mrefu, TAZARA imekuwa ikitazamwa kama mpinzani wa Ukanda wa Lobito—mradi unaofadhiliwa na Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya kuunganisha Angola, Zambia, na DRC.

