Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye, amefanya mabadiliko madogo katika Serikali yake kwa kuteua Mawaziri wapya katika Wizara mbalimbali muhimu za nchi.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, mabadiliko hayo yamegusa Wizara ya Habari na Mawasiliano, Wizara ya Miundombinu pamoja na Wizara ya Afya, hatua inayoonekana kuendeleza mchakato wa mageuzi ya Uongozi ndani ya taasisi za Serikali.
Katika uteuzi huo, Balozi Evelyne Butoyi, aliyekuwa akihudumu kama Balozi wa Burundi nchini Zambia, amerejeshwa nyumbani na kuteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Vyombo vya Habari. Anachukua nafasi ya Gabby Bugaga, aliyefariki dunia hivi karibuni kufuatia ajali iliyotokea usiku wa tarehe 15 kuamkia 16 Aprili mwaka huu.
Kwa upande wa Wizara ya Miundombinu, Ujenzi, Usafirishaji wa Watu na Mizigo pamoja na Vifaa, Mhandisi Egide Nijimbere ameteuliwa kuwa Waziri mpya, akichukua nafasi ya Damien Niyonkuru ambaye alikuwa ameteuliwa mapema mwaka huu.
Aidha, katika Wizara ya Afya, Dkt. Fidèle Nkezabahizi ameteuliwa kushika wadhifa huo, akimrithi Lidwine Baradahana. Kabla ya uteuzi huo, Nkezabahizi alikuwa akiongoza Mradi wa kitaifa unaohusiana na lishe na afya bora.
Mabadiliko hayo yanajiri wiki chache baada ya Rais Ndayishimiye kufanya mabadiliko mengine katika sekta ya Jeshi, jambo linaloashiria mwendelezo wa juhudi za kuimarisha uongozi na utendaji wa taasisi za Serikali nchini Burundi.

