Paris Saint-Germain wapanda kwa muda kileleni mwa msimamo wa Ligue 1 baada ya ushindi wa kusuasua wa mabao 3-2 dhidi ya klabu ya Metz.
Mabingwa hao walipata mabao yao kupitia Gonçalo Ramos, Quentin Ndjantou na Désiré Doué, lakini walilazimika kupambana hadi mwisho baada ya Metz kupunguza tofauti ya mabao mara mbili.
Kwa ushindi huo, PSG wamefikisha pointi 36, wakiwa mbele kwa pointi mbili dhidi ya Lens watakaocheza na Nice Jumapili. Metz wanaendelea kubaki mkiani mwa ligi wakiwa na pointi 11 pekee.
PSG walipata bao la kwanza dakika ya 31 baada ya Lee Kang-in kuanzisha mpira wa kona fupi kabla ya kuinua mpira uliomkuta Ramos, ambaye aliupiga kichwa na kuutumbukiza wavuni. Dakika nane baadaye, Ibrahim Mbaye alitoa pasi safi ndani ya boksi na Ndjantou akaifunga kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na PSG, akiwa mchezaji wa 17 tofauti kufunga kwa PSG msimu huu wa Ligue 1.
Hata hivyo, dakika chache kabla ya mapumziko, Metz walipata bao la kujifariji kupitia Jessy Deminguet, aliyepiga shuti kali baada ya mpira uliotemwa ndani ya boksi.
Kipindi cha pili kilikuwa na presha kubwa kwa PSG licha ya nafasi kadhaa walizopata. Metz walikaribia kusawazisha, lakini kipa wa PSG Matvey Safonov aliokoa michomo hatari. Dakika ya 63, PSG walipiga shambulizi la kushtukiza na Désiré Doué akafunga bao la tatu kwa utulivu mkubwa.
Metz hawakukata tamaa na dakika tisa kabla ya mwisho walifunga bao la kuvutia kupitia Giorgi Tsitaishvili, aliyemalizia pasi ya kisigino ya Gauthier Hein, na kuifanya mechi iwe ya presha kubwa kwa PSG hadi filimbi ya mwisho.
PSG waliweza kushikilia ushindi huo, lakini Metz walionyesha dalili za matumaini. Ikiwa wataendelea kucheza kwa kiwango hiki dhidi ya wapinzani wa daraja lao, bado wana nafasi ya kuepuka kushuka daraja kwenda Ligue 2.

