Atakribani watu 28, wakiwemo wanafunzi 27 na mwalimu mmoja, wamepoteza maisha kufuatia mkasa wa kuporomoka kwa paa la shule huko Peshawar, nchini Pakistan. Taarifa hizi za kusikitisha zimethibitishwa na Msemaji wa Hospitali ya Lady Reading, Mohammad Asim, ambaye ameeleza kuwa ajali hiyo imesababisha maafa makubwa kwa jamii ya eneo hilo.
Mbali na vifo hivyo, msemaji huyo alibainisha kuwa watu wengine 19 wamepata majeraha mbalimbali, ambapo watano miongoni mwao wapo katika hali mahututi. Majeruhi wengi waliopokelewa hospitalini hapo wameripotiwa kuwa ni watoto wadogo waliobainika kupata majeraha mabaya ya kichwani.
Matokeo ya ajali hiyo yalisababisha taharuki kubwa iliyowafanya wazazi wengi kumfurika hospitalini hapo kutafuta taarifa za watoto wao. Ili kuweka mambo sawa na kuzuia msongamano mkubwa, uongozi wa hospitali hiyo ulilazimika kuomba msaada wa jeshi la polisi ili kudhibiti umati na kuruhusu huduma za uokoaji kuendelea. Mohammad Asim aliongeza kuwa watoto walioathiriwa na janga hili wana umri wa kati ya miaka 6 na 12.
Kufuatia msiba huo, Rais wa Pakistan, Asif Ali Zardari, kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi yake kwenye mtandao wa X, ameeleza kushtushwa na kusikitishwa sana na vifo pamoja na majeraha yaliyowapata wanafunzi na walimu. Alisisitiza kuwa msiba huo wa kuhuzunisha umeigusa na kuishtua nchi nzima.Mwisho, Rais Zardari ametuma salamu za rambirambi na pole za dhati kwa familia za wahanga.Pia, amewaombea waliookoka wapone haraka na kikamilifu, huku akiagiza mamlaka zinazohusika kuhakikisha majeruhi wote wanapata huduma bora na za haraka za matibabu.
