Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ametangaza vikwazo dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), hatua iliyotajwa katika taarifa hiyo kuashiria kuongezeka kwa mvutano kati ya Serikali ya Marekani na Mahakama hiyo ya Kimataifa.
Tangazo hilo lilitolewa siku ya Ijumaa, saa chache baada ya Tuzo ya Nobel kutolewa kwa Navi Pillay, aliyewahi kuhudumu kama Jaji wa Mahakama hiyo.
Akizungumzia hatua hiyo, Rubio aliitaja ICC kuwa ni “Mahakama iliyopotoka” na kutishia kuchukua hatua zaidi za kusambaratisha.
Rubio alisema Marekani inalenga “kuivunja vipande vipande hatua kwa hatua,” kauli inayoashiria msimamo mkali wa Serikali yake dhidi ya taasisi hiyo ya Kimataifa.
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), yenye Makao yake Makuu jijini The Hague, Uholanzi, ina jukumu la kuwafungulia Mashtaka na kuwahukumu watu wanaotuhumiwa kutenda uhalifu mkubwa wa Kimataifa, ikiwemo mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binadamu, uhalifu wa kivita na uhalifu wa uchokozi, kwa kuzingatia Mamlaka yake ya kisheria.
Hatua ya Marekani dhidi ya ICC inaibua maswali kuhusu uhusiano kati ya Washington na taasisi za Kimataifa zinazohusika na uwajibikaji wa kisheria.

