Uongozi wa Iran umekubali pendekezo la kusitisha mapigano kwa kipindi cha wiki mbili, hatua inayotajwa kuwa sehemu ya juhudi za Kidiplomasia za kupunguza mvutano kati ya Iran na Marekani.
Taarifa hiyo inafuatia tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump ambaye alisema amekubaliana kusimamisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa muda wa siku 14, akieleza kuwa hatua hiyo ni “sitisho la mapigano pande zote mbili.” 
Kwa mujibu wa vyanzo vya Kidiplomasia, makubaliano hayo yalifikiwa baada ya mazungumzo yaliyosimamiwa na Pakistan, ambapo viongozi wa nchi hiyo walifanya mazungumzo ya moja kwa moja na Washington pamoja na Tehran ili kuzuia kuongezeka kwa vita katika eneo la Mashariki ya Kati. 
Pendekezo hilo linajumuisha kusimamishwa kwa mashambulizi ya kijeshi kwa muda wa wiki mbili huku pande zote zikipewa nafasi ya kuendelea na mazungumzo ya amani ya kudumu. Aidha, suala la kufunguliwa kwa njia ya bahari ya Strait of Hormuz limepewa uzito mkubwa katika mazungumzo hayo kutokana na umuhimu wake kwa biashara ya mafuta duniani. 
Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema hatua hii inaweza kuwa mwanzo wa makubaliano ya amani ya muda mrefu ikiwa pande zote zitaheshimu masharti yaliyowekwa.

