Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo amesema Mamlaka hiyo imekamata aina mbalimbali ya madawa ya kulevya kupitia operesheni iliyofanyika.
Amesema kuwa pamoja na mambo mengine, mamlaka hiyo pia imebaini mbinu ambayo baadhi ya wahalifu wa biashara ya dawa za kulevya ambao hutumia maiti za binadamu kama mifuko ya kubebea dawa hizo haramu.
Katika operesheni hiyo, amesema kuwa mamlaka imewakamata watu wawili waliokuwa wamiliki wa kiwanda bubu kilichokuwa kikitengeneza biskuti zilizochanganywa na bangi katika eneo la Sinza jijini Dar es Salaam, ambazo zilikuwa zikisambazwa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Lindi na Mtwara.
Amesema katika operesheni kubwa zilizofanyika kuanzia mwezi Mei hadi Julai mwaka huu, mamlaka yake kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 37,197.142 za dawa za kulevya za aina mbalimbali.
Dawa hizo ni pamoja na kilogramu 11,031.42 za Mitragyna Speciosa (Kratom), bangi kilogramu 24,873.56, mirungi kilogramu 1,274.47, skanka kilogramu 13.42, heroin kilogramu 2.21 na methamphetamine gramu 1.42, pamoja na dawa tiba zenye asili ya kulevya zikiwemo ketamine kilogramu 1.92, vidonge 1,000 vya Rohypnol na lita 6 za hydrochloric acid.
Katika operesheni maalum iliyofanyika bandari kavu ya Temeke jijini Dar es Salaam, amesema mamlaka hiyo ilikamata kilogramu 11,031.42 za Mitragyna Speciosa kutoka Sri Lanka, zilizokuwa zimefichwa kwenye mifuko iliyoandikwa kuwa ni mbolea.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema mmea huo una kemikali hatari zinazoweza kuathiri mfumo wa fahamu na kusababisha uraibu na vifo vya ghafla.
Vilevile, raia wawili wa China, Chein Bai na Qixian Xin, walikamatwa katika eneo la Posta jijini Dar es Salaam wakiwa na methamphetamine gramu 1.42, Rohypnol vidonge 1,000 na ketamine kilogramu 1.92.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema katika kipindi hicho pia, DCEA iliteketeza ekari 1,045.5 za mashamba ya bangi katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Mara, Kagera, Dodoma, Tabora, Morogoro na Arusha, huku ikikamata dawa za mashambani zenye uzito wa kilogramu 26,191.45.

