Kompany Kusubiri Dakika za Mwisho Kumtumia Harry Kane Dhidi ya Real Madrid

Kompany Kusubiri Dakika za Mwisho Kumtumia Harry Kane Dhidi ya Real Madrid

Kocha wa Bayern Munich, Vincent Kompany, ameweka kitendawili kuhusu ushiriki wa nahodha wa Uingereza, Harry Kane, katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) dhidi ya Real Madrid kesho Jumanne. Licha ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 32 kufanya mazoezi na kikosi siku ya Jumatatu baada ya kupona jeraha la kifundo cha mguu lililomuweka nje ya michezo ya kimataifa mwezi uliopita, Kompany amesisitiza kuwa uamuzi wa mwisho utatolewa saa chache kabla ya mtanange huo kuanza pale Bernabéu.

Kurejea kwa Kane itakuwa ni habari njema kwa mabingwa hao mara sita wa Ulaya, kwani amekuwa na msimu wa kimbunga akifunga mabao 48 katika michezo 40 msimu huu. Kompany ameeleza kuwa Kane hajaoteza mahadhi ya mchezo licha ya kukosa ushindi wa hivi karibuni wa Bayern wa 3-2 dhidi ya Freiburg, na kwamba kikosi chake kiko imara na tayari kwa mapambano hayo, huku kipa Sven Ulreich pekee akiwa ndiye mchezaji asiyepatikana. Bayern inaingia Madrid ikiwa na fomu nzuri, ikiongoza Bundesliga kwa alama tisa, tofauti na Real Madrid ambao bado wanauguza maumivu ya kichapo cha Mallorca mwishoni mwa wiki.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Madrid, beki huyo wa zamani wa Manchester City amekiri kuwa kuikabili Real Madrid ugenini ni moja ya mitihani migumu zaidi katika soka, lakini amewataka wachezaji wake kucheza bila uoga. Kompany amebainisha kuwa mchezo huo utaamuliwa na mbinu pamoja na ubora wa mchezaji mmoja mmoja, huku akisisitiza kuwa Bayern imejifunza mengi kutokana na jinsi Real walivyowaondoa Manchester City katika hatua iliyopita. Ulimwengu wa soka unasubiri kuona kama “Mnyama” Harry Kane atapewa nafasi ya kuongoza mashambulizi na kuendeleza rekodi yake ya ufungaji dhidi ya miamba hiyo ya Hispania.

Comments

No comments yet. Why don’t you start the discussion?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *