Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Mary C. Levira amesema kuwa Chuo kina jukumu kubwa katika kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na kutoa wito kwa Uongozi pamoja na Watumishi kuhakikisha mipango ya Chuo inaendana na malengo ya taifa.
Amesema hayo wakati akifungua Kikao cha Kwanza cha Baraza la Tano la Wafanyakazi wa IJA kilichofanyika Chuoni Lushoto April 09, 2026.
“Tunapaswa kuhakikisha shughuli zetu zote zinaendana na Dira ya Taifa. Hii inahusisha ubunifu, matumizi ya teknolojia, pamoja na kuimarisha rasilimali watu ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye,” amesisitiza.
Pia amesema: “Vikao kama hivi vinaipa taasisi fursa ya kupokea maoni kutoka kwa Watumishi, maoni ambayo husaidia Baraza la Uongozi kufanya maamuzi sahihi linapopokea hoja mbalimbali kutoka kwa watumishi.”
Kabla ya kikao hicho, wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi walipatiwa mafunzo ya maarifa ya kifedha (Financial literacy) pamoja na utambuzi wa fursa mbalimbali za uwekezaji ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwaongezea maarifa katika matumizi sahihi ya fedha na kutambua miradi yenye tija katika uwekezaji.
Akizungumzia mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, amesema yanalenga kuwajengea uwezo Watumishi katika masuala ya kifedha na uwekezaji.
“Lengo ni kuwawezesha watumishi kuelewa matumizi sahihi ya fedha, umuhimu wa kuweka akiba, maeneo sahihi ya kuwekeza, na namna bora ya kutumia mikopo kwa tija,” amesema Mhe. Dkt. Kihwelo.
Mafunzo hayo yamewezeshwa na Mtaalamu wa Huduma za Dhamana kutoka Benki ya NMB, Bw. Baltazary Tarimo, ambaye aliwashauri washiriki kuwekeza katika maeneo mbalimbali, ikiwemo hisa na hatifungani, ili kuongeza kipato chao kwa manufaa ya sasa na ya baadaye.
Naye Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Taasisi za Habari, Vyuo vya Ufundi Stadi na Taasisi za Utafiti (RAAWU) Kanda, Bw. Bwake Mwaisemba, ameupongeza uongozi wa IJA kwa kushughulikia kwa ufanisi na kwa wakati changamoto za wafanyakazi.
Pia amesifu ushirikiano mzuri uliopo kati ya Uongozi wa Chuo na RAAWU bila kuwepo kwa migogoro.

