Hali ya usalama katika ukanda wa Mashariki ya Kati imeingia katika hatua ya hatari zaidi mnamo Machi 18, 2026, kufuatia shambulio kubwa dhidi ya shamba la gesi la Pars nchini Iran ambalo limeibua tishio la vita vya nishati duniani kote. Shambulio hilo lililolenga matangi ya kuhifadhia gesi na sehemu ya kinu cha kusafishia, limesababisha moto mkubwa na kupelekea wafanyakazi kuhamishwa kwa dharura, huku vyombo vya habari nchini Israel vikiripoti kuwa oparesheni hiyo imefanywa na jeshi la Israel kwa ridhaa ya Marekani. Tukio hili limekuwa ni kichocheo kikubwa cha kupanda kwa bei ya mafuta ya Brent ambayo imepaa kwa asilimia 5 na kufikia zaidi ya dola 108 kwa pipa, hali inayotikisa masoko ya hisa na uchumi wa dunia kwa ujumla.
Katika hatua ya kulipiza kisasi, serikali ya Tehran imetoa tamko kali ikitaja vituo vikuu vya mafuta na gesi katika nchi za Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), na Qatar kuwa ni “shabaha halali na za moja kwa moja” za mashambulizi yake yajayo. Iran imetoa onyo la mwisho ikizitaka nchi hizo kuwahamisha wafanyakazi wao mara moja kutoka kwenye maeneo nyeti kama kinu cha Samref nchini Saudi Arabia, shamba la gesi la Al Hosn nchini UAE, na kinu cha Ras Laffan nchini Qatar kabla ya makombora kuanza kurushwa katika saa chache zijazo. Hatua hii inakuja wakati Iran ikiwa tayari imefunga Mlangobahari wa Hormuz, njia inayopitisha asilimia 20 ya nishati duniani, jambo ambalo limezifanya nchi za Qatar na UAE kulaani shambulio hilo dhidi ya Iran zikidai kuwa ni kitendo cha hatari kinachochezea usalama wa nishati ya kila mwananchi duniani.

