Klabu ya Brighton & Hove Albion imechukua hatua kubwa katika juhudi za kumsajili winga machachari wa FC Koln, Said El Mala (19), huku ikiripotiwa kuwa tayari kuweka rekodi mpya ya usajili kwa klabu hiyo ya Ujerumani.
Baada ya kufuatilia maendeleo ya kijana huyo kwa miezi tisa, Brighton wanajiandaa kuwasilisha ofa ya €35 milioni (pamoja na bonasi za ziada). Kinachowapa Brighton nafasi kubwa zaidi kuliko washindani wao ni utayari wao wa kuwasajili ndugu wawili kwa mpigo: Said na kaka yake, Malek El Mala (20).
Mama mzazi wa wachezaji hao, Sabrina, ambaye sasa ndiye mwakilishi wao kisheria (agent), tayari ametoa baraka zake kwa mazungumzo hayo kuendelea.
Vigogo wa EPL Wataharuki
Mabadiliko ya uwakala wa Said yamevutia macho ya klabu kubwa duniani. Mbali na Brighton, klabu zifuatazo zimeanza mawasiliano na mkurugenzi wa Koln, Tim Steidten:
- Chelsea: Wameripotiwa kuwasiliana moja kwa moja na uongozi wa Koln.
- Manchester City: Wanafuatilia kwa ukaribu ukuaji wa kasi wa kinda huyo.
- Bayern Munich: Miamba hiyo ya Ujerumani pia haitaki kupitwa na talanta hiyo ya nyumbani.
Licha ya shinikizo hilo, Mkurugenzi wa Michezo wa Koln, Thomas Kessler, amesisitiza kuwa klabu hiyo haina haraka. Said ana mkataba mrefu hadi mwaka 2030 usio na kipengele cha kumruhusu kuondoka kwa bei rahisi (release clause).
Kocha wa Koln, Lukas Kwasniok, amesifu uwezo wa Said akibainisha kuwa tayari amefunga mabao 10 msimu huu, licha ya mara nyingi kutokea benchi kama mchezaji wa akiba.

