Barcelona imekumbwa na jinamizi lingine nyumbani baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Atletico Madrid katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) uliopigwa Jumatano usiku. Licha ya Barcelona kutawala mchezo kwa muda mrefu, kadi nyekundu ya beki chipukizi Pau Cubarsi katika dakika ya 42 ilibadili mwelekeo wa mchezo na kuwapa nafasi vijana wa Diego Simeone kutawala uwanja wa Camp Nou.
Mshambuliaji Julian Alvarez aliwastaajabisha mashabiki wa Catalan kwa kufunga bao la kwanza kwa mkwaju wa faulo wa umbali wa mita 25 uliotinga moja kwa moja kwenye kilele cha nyavu sekunde chache kabla ya mapumziko. Bao hilo lilikuja kufuatia rafu ya Cubarsi dhidi ya Giuliano Simeone, ambapo mwamuzi aliondoa kadi ya njano na kutoa nyekundu baada ya mapitio ya VAR, akiamini Cubarsi alikuwa mchezaji wa mwisho.
Katika kipindi cha pili, kocha Hansi Flick alijaribu kufanya mabadiliko huku Marcus Rashford akigonga mwamba kwa faulo, lakini nidhamu ya ulinzi ya Atletico ilikuwa kuta ya zege. Katika dakika ya 70, Atletico walizidisha maumivu kwa Barca pale Matteo Ruggeri alipopiga krosi safi iliyomkuta Alexander Sorloth, ambaye aliunganisha mpira huo nyavuni na kuifanya score iwe 2-0.
“Tumevunjika moyo, lakini ninaamini tunaweza kupindua matokeo haya katika mchezo wa marudiano. Kipindi cha pili tulicheza kwa nguvu licha ya kuwa pungufu,” alisema beki wa Barca, Ronald Araujo.
Ushindi huu wa ugenini unawapa Atletico faida kubwa kuelekea mchezo wa marudiano wiki ijayo mjini Madrid. Mshindi wa jumla wa pambano hili atavaana na mshindi kati ya Arsenal au Sporting CP katika hatua ya nusu fainali. Kwa Barcelona, sasa wanalazimika kushinda kwa mabao matatu ugenini ili kusonga mbele, jambo ambalo ni mlima mrefu kupanda dhidi ya ulinzi thabiti wa Simeone.

