Ubalozi wa Urusi nchini Sudan umesema unachunguza ripoti kwamba ndege ya mizigo iliyokuwa na wafanyakazi wa Urusi ilidunguliwa huko Darfur, uwanja muhimu wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya jeshi na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF).
Ndege hiyo, iliyotambulika kama ilyushin Il-76 iliyotengenezwa nchini Urusi, ilikuwa kwenye misheni ya kupeleka vifaa na dawa katika mji unaoshikiliwa na jeshi wa el-Fasher, duru za kijeshi ziliambia vyombo vya habari vya Sudan.
Siku ya Jumatatu, RSF ilisema iliiangusha ndege iliyotengenezwa Urusi iliyokuwa ikisafirishwa na jeshi la Misri ambayo ilishutumu kwa kuwalipua raia – ingawa ilitambuliwa kama Antonov.
Misri imekanusha shutuma kwamba imekuwa ikitoa msaada wa kijeshi kwa jeshi la Sudan wakati wa mzozo uliodumu kwa miezi 18.

