Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imevitaka vyombo vya habari nchini kuhakikisha vinazingatia weledi kwa kuripoti kwa usahihi taarifa zote zinazohusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kwa kufanya hivyo, watawapa wananchi taarifa sahihi zinazohusu Uchaguzi na kushiriki kikamilifu.
Kauli hiyo imetolewa leo, tarehe 1 Agosti 2025, jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, wakati wa ufunguzi wa mkutano kati ya Tume na Wahariri wa Vyombo vya Habari.
Jaji Mwambegele amesema vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya mpiga kura na taarifa sahihi zinazowawezesha kufanya maamuzi ya msingi kwa uhuru na kwa amani.
Aidha, amewasihi Wahariri wa vyombo vya habari kutumia majukwaa yao kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu, utakayofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.

