Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, ameweka mazingira ya kitendawili kuelekea mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Southampton utakaopigwa Jumamosi hii, huku kukiwa na uwezekano wa kurejea kwa nyota muhimu. Licha ya kuthibitisha kuwa winga wa kimataifa wa Uingereza, Noni Madueke, ataikosa mechi hiyo kutokana na jeraha la goti alilolipata akiwa na timu ya taifa, Arteta ametoa mwanga wa matumaini kuhusu kurejea kwa nahodha Martin Odegaard na beki Jurrien Timber. Madueke alikuwa miongoni mwa kundi kubwa la wachezaji 11 wa Arsenal waliojiondoa kwenye majukumu ya kimataifa mwezi uliopita kutokana na majeraha, hali inayozua presha kubwa wakati klabu hiyo ikipambana kutwaa ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu tangu mwaka 2004.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Ijumaa, Arteta amesisitiza kuwa maamuzi ya wachezaji wake kutochezea timu zao za taifa yalizingatia ushauri wa kitaalamu wa kitabibu na si vinginevyo. Amesema anajivunia kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wanaoitwa kwenye timu za taifa na kwamba klabu imekuwa ikiwapa ushirikiano mkubwa, lakini kwa sasa kipaumbele ni kuhakikisha kikosi kinakuwa na utimamu kuelekea hatua hizi za mwisho za msimu. Habari njema kwa mashabiki wa “The Gunners” ni kwamba jeraha la Madueke halionekani kuwa baya kama lile lililomweka nje kwa wiki sita huko nyuma, ingawa bado hatahusika katika mchezo wa kesho.
Kuelekea mchezo huo utakaopigwa katika uwanja wa St Mary’s, Arsenal inatafuta namna ya kurejesha furaha ya mashabiki wake baada ya kupoteza fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Manchester City mwezi uliopita. Licha ya wachezaji kama William Saliba, Gabriel Magalhaes, Bukayo Saka, na Declan Rice kukosa michezo ya mataifa yao, Arteta amegoma kuweka wazi ni nani kati yao atakuwa fiti kuanza kesho. Kocha huyo amesisitiza kuwa wako katika nafasi ambayo wanahitaji kupanga kikosi chenye nguvu zaidi ili kushinda kila mashindano yaliyosalia, akibainisha kuwa Kombe la FA lina umuhimu wa kipekee kwa klabu hiyo yenye rekodi ya kutwaa taji hilo mara nyingi zaidi nchini Uingereza.

