WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafirishaji wa majini ili kukuza biashara, kuunganisha masoko na kuongeza mchango wa bara hilo katika uchumi wa dunia.
Amesema maendeleo ya sekta hiyo ni muhimu katika kuunganisha nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini, akisisitiza kuwa ushirikiano wa kiuchumi ni miongoni mwa njia muhimu za kuimarisha umoja wa Waafrika na kutimiza ndoto za waasisi wa bara hilo.
Dkt. Nchemba ameyasema hayo katika Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri la Shirika la Usafiri wa Majini la Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini (Maritime Organisation for Eastern, Southern and Northern Africa (MOESNA), uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, ambapo amebainisha kuwa Tanzania ina nafasi muhimu katika kufanikisha azma hiyo kutokana na jiografia yake, ikipakana na Bahari ya Hindi na kuwa na maziwa makubwa yakiwemo Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa itifaki ya kikanda ya usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya majini pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa ushirikiano baina ya kampuni za meli za kikanda, akieleza kuwa hatua hizo zitasaidia kuimarisha biashara na kupunguza changamoto za usafirishaji zinazokabili nchi za bara hilo.
Aidha, Dkt. Nchemba amesema maendeleo ya usafirishaji wa majini yanapaswa kwenda sambamba na uwekezaji katika miundombinu ya reli na barabara ili kuunganisha bandari, masoko na nchi jirani, akibainisha kuwa hatua hizo zinaendana na malengo ya Agenda ya Afrika 2063 na Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).
Amesema mkutano huo ni fursa ya kupitia mafanikio na changamoto za sekta hiyo na kuweka maazimio mapya yatakayotekelezeka kwa manufaa ya nchi wanachama, huku akiwakaribisha wajumbe kutoka nchi mbalimbali nchini Tanzania na kuwataka kutumia nafasi hiyo kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya uchukuzi wa majini, ikiwemo kuendeleza mafunzo ya wataalamu na maandalizi ya chuo cha kikanda cha usafirishaji wa majini ili kuongeza ujuzi na uwezo wa nchi wanachama.
Profesa Mbarawa amesema utekelezaji wa mipango hiyo utasaidia kuongeza upatikanaji wa meli zenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya usafirishaji wa mizigo na abiria, kupunguza utegemezi wa njia za usafirishaji kutoka maeneo ya mbali na kuimarisha biashara ya kikanda, huku akisisitiza umuhimu wa usalama wa majini na kukabiliana na vitisho vinavyoweza kuathiri shughuli za usafirishaji.
